Siri 5 Za Ndoa Usizozijua
Ndoa ni tamu asikwambie mtu, ni maneno ya kwanza niliyoambiwa na Mama yangu siku nilipomwambia kuwa kuna watu wanataka kuja kuleta posa nyumbani. Kama Mama alifurahi kuwa nimepata mwenza ambae nitaenda kuanza nae maisha.
Baada ya shughuli za barua ya posa kuletwa na tarehe ya mahari kupangwa mambo yalizidi kuwa moto kwa Mama yangu na mdogo wangu, walianza kupanga mipango mingi ya sherehe na kila kitu wakati Mimi nilikuwa nachukulia ni kitu cha kawaida sana.
Siku chache kabla ya mahari kuletwa, Mama yangu akaniita na kuniambia, mwanangu unaenda kuanza maisha mapya ya ndoa kwa hilo nakutakia heri zote lakini nataka nikwambie mambo 5 muhimu yatakayo kusaidia Wewe na mwenzio kuwa na ndoa yenye amani na furaha. Baada ya kusema hayo akaniambia Maanti zako wanakuja ili wote tuongee na wewe pamoja.
Walivyofika baada ya salamu na kila kitu wakaniambia, tutakwambia mambo 5 tu muhimu ambayo tunauhakika uyafahamu kuhusu ndoa lakini ni ya muhimu sana.
Jambo la 1
Kufanya mapenzi na mwenzio ni muhimu na sio tu unafanya umalize unaiweka akili yako na hisia zako hapo kwani mara nyingi wakati wa tendo au mnapomaliza tendo huwa kuna kuongea na mawasiliano ni muhimu sana baina yenu. Kwahiyo usiache kumpa mwenzio tendo au kuchochea tendo la ndoa muhimu.
Jambo la 2
Heshimu Faragha ya Mwenzako
Mwenzio akiwa anaongea na simu na wazazi wake au ndugu zake, kuna namna ambavyo ameshazoea kuongea na wanaweza muuliza kitu akajihisi aibu kujibu mbele yako, kwahiyo hili nalo uzingatie.
Jambo la 3.
Uwe na mipaka
Hapa walimaanisha kwamba uwe unachagua aina ya maneno ya kumwambia mwenzio hata kama umekasirika, usiropoke tu kwakuwa una hasira chagua maneno ili kuepusha kuja kujutia baadae.
Jambo la 4.
Suala la kuonyesha hisia
Inawezekana mwenzio sio mtu wa kupenda au hajazoea kuonyesha hisia zake waziwazi hasa mnapokuwa mbele ya kadanamsi, lakini haimaanishi kuwa hakupendi ni jinsi alivyo, kwahiyo inabidi umsome na umwelewe. Kama kwake ni kitu kigumu usimlazimishe, unaweza ukaanza kumwelekeza polepole.
Jambo la 5.
Fahamu namna ya kutenganisha muda wa kazi zako, mume na watoto. Hapa kila kitu kinahitaji umakini na muda wako basi usiache kimoja au viwili vikaelemewa.
Haya ndio mambo 5 muhimu ambayo tunataka uyajue, na unaweza kudhani ni ya kipuuzi au sio ya maana sana lakini ukiyazingatia ndoa yako utaifurahia na itakuwa na amani.
Baada ya kumaliza kuambiwa haya nilishusha pumzi kwanza kwasababu kwangu ni vitu ambavyo sikutegemea lakini nikajiambia kuwa nitavifuata ili nijihakikishie je ni ya kweli haya?
Baada ya kufunga ndoa nilianza kufuata ushauri huu pamoja na mingine niliyopewa siku ya Kitchen party na nimejidhihirisha kuwa nilichoambiwa kweli kimefanya kazi na kinaendelea kufanya kazi, kwani ndoa sasa ina miaka 6 na kilicho ndani ya ndoa yetu ni amani, upendo na furaha ya kweli.
Hizi ndio siri tano za ndoa ambazo nilikuwa sizijui ila sasa Mimi na wewe wote tunazijua.