Kama Hii Ilishakutokea Mshukuru Sana Mungu

Lilian Chonya
3 min readFeb 21, 2022

--

Leo katika harakati zangu za maisha ya kila siku ili kuhakikisha naendelea kuifanya familia yangu ile, ivae vizuri na kuishi mahali salama, nikakutana na mdada mmoja kwenye bajaji ya kuchangia ana lalamika sana kwenye simu huku machozi yanamtoka.

Ndani ya bajaji tulikuwepo watu watatu tu, Mimi, Yeye na dereva ambaye naye alikuwa yuko busy na kazi yake kwahiyo hata kilichokuwa kinaendelea huku nyuma hakukijua. Wakati naendelea kumtafakari huyu dada na maneno ya uchungu ambayo alikuwa anaongea na huyu mtu mwingine wa upande wa pili kwenye simu, ghafla nikaisikia simu yangu inaita na ikanitoa kutoka katika mawazo niliyokuwa nayo kwa wakati huo.

Baada ya kumaliza kuongea na simu yangu, nikamwangalia huyo dada wa pembeni yangu ili nimsabahi nikakuta amejifunika usoni na mtandio wa kijora chake cha rangi ya chuichui alichokuwa amevaa. Nikataka nimguse bega lakini mkono wangu ukawa mzito ila kwakuwa bado alikuwa analia kwa sauti ndogo na ya chini nikajikaza na kumgusa begani. Wakati nataka kumsalimia nikashangaa maneno ambayo nilikuwa nimepanga kuanza nayo yamepotea na kuanza kumwambia moja kwa moja kuwa pole usilie sana ndoa zina changamoto sana.

Aliniangalia na kuanza kulia tena, nikaishiwa maneno na wakati natafakari nini cha kusema akaanza kuniambia yaani Mimi huyu mwanaume nimemvumilia katika mengi sana,nimemsaidia sana, nimejitoa kwake sana ila leo hii maisha yameshakaa kwenye mstari ananiambia hawezi kunioa kwasababu wazazi wake wamekwisha mtafutia mwanamke mwingine hivi kweli? Hapo mbona nilishusha pumzi kwa nguvu na nikaishiwa pozi kwasababu kwa kumwangalia tu huyu dada anaonekana ni wale wadada wapambanaji.

Baada ya ukimya kama wa dakika tano kabla sijaanza kuongea bajaji ikasimama na abiria mwingine akaingia alikuwa ni Mama mtu mzima tukamsalimia na safari ikaanza tena. Yule dada akachukua tena mtandio wake akajifunika usoni na kuanza kulia tena kwa sauti ya chini. Nikambonyeza begani na kumwambia najua una uchungu lakini je umeshajaribu kuongea nae huyu mwanaume ili upate kusikia kauli yake ya mwisho kuhusu hili swala? Akasema yaani hapa nimetoka kwake na bado anakazania kuwa ndoa na Mimi haitawezekana hawezi kwenda kinyume na matakwa ya wazazi wake.

Nimembeleleza sana na nikamkumbusha tulipotoka kwasababu tumekuwa wote kwa miaka 5, lakini amesema haiwezekani Mimi nitafute tu mtu mwingine niendelee na maisha yangu. Akasema inaniuma kwasababu nyumbani kwetu wote wanamfahamu na wanajua ndio atakuja kunioa, lakini ona sasa nitaenda kuwaambia nini wazazi na ndugu zangu?

Mara yule Mama wa makamk aliyepanda akatugeukia na kusema mwanangu si bora umshukuru Mungu badala ya kulia kwasababu kwanza hujui amekuepusha na nini huko mbele ya safari, na pili huyo hakuwa wa kwako kwasababu laiti angekuwa ni wako ambaye Mungu amekuandalia basi asingefanya hayo. Akasema hebu fikiria kama mngefunga ndoa na miaka miwili ndani ya ndoa unaanza kugundua ana mahusiano na wanawake wengine huko nje, ungejisikiaje na hapo labda una mtoto tayari?

Mshukuru Mungu hili limetokea mapema kwasababu Mungu amekwisha kuandalia mtu wako na yupo, huyo ametumika kama daraja la kukusaidia Wewe kwenda kumfikia aliye wako kiroho na kihisia. Usipoteze muda wako kulia lia unapoteza Machozi yako. Baada ya kusema hayo yule Mama akamwambia dereva wa bajaji amshushe kituo cha mbele kwani amefikia.

Baada ya yule Mama kushuka nikamwamgalia yule dada tena, nikakuta ameacha kulia na anatoa miwani yake ya jua kwenye pochi ili aivae. Kisha akaniambia huyu Mama ameniambia mambo ya msingi sana siwezi kuendelea kumlilia mtu ambae sio wa kwangu kuanzia sasa hivi nitakuwa namshukuru Mungu tu. Yote ambayo niliweza kujifunza wakati nipo naye nitayatumia katika maisha yangu, nitaendelea kupambana ili atakapokuja wa kwangu anikute nimeshajiandaa tuanzie pale ambapo kila mmoja atakuwa amefikia.

Kiukweli nilishangaa kuona mabadiliko hayo ya ghafla kutoka kwake na kabla sijasema chochote dereva wa bajaji akatugeukia na kusema tumefika mwisho wa safari naomba nauli, kila mtu akatoa nauli yake tukashuka na wote tukaendela na mishe zetu za siku hiyo. Wakati natembea nikawa nayatafakari sana maneno ya yule Mama yalikuwa ni machache lakini yaliyobeba ujumbe mkubwa ndani yake. Nikagundua kumbe ni kweli kuna wakati mtu unaweza kuwa unang'ang'ania kitu au mtu na sio wako au chako. Nikakumbuka mengi sana lakini nikajikumbusha na maneno ya yule mama kuwa mshukuru Mungu kwakuwa hujui amekuepusha na kitu gani huko mbele.

--

--

Lilian Chonya
Lilian Chonya

Written by Lilian Chonya

Karibu usome nakala zangu kuhusu| Mahusiano | Malezi | Ndoa

No responses yet