Kama Hakujali Kimwili, Hawezi Kukujali Kiroho.

Lilian Chonya
3 min readMar 16, 2022

--

Majuzi katika pita pita zangu katika mtandao mmoja, nikakutana na post ya mdada mmoja ambaye anaomba msaada wa kisheria ili aweze kutengana na Mume wake kwasababu amechoka kupigwa kila siku. Kama kawaida watu wakawa wanakomenti pale kumlaani na kumtukana yule mwanaume. Katika kusoma zile komenti sikuona hata moja ambayo inamuulize yule dada maswali magumu(labda kwasababu wengi waliokuwa wanakomenti ni wanawake)nikaishia hapo kuendelea na mambo yangu mengine.

Baadae nikaanza kutafakari tena hilo swala la huyo mdada na kwa siku mbili mfululizo nilikuwa najiuliza maswali mengi sana, mengine nikapata majibu, mengine nikayatuma kwa watu wengine ili nao waniambie majibu na mawazo yao. Baada ya kupitia majibu yote, nikagundua vitu kadhaa ambavyo wengi tunavipuuzia lakini ni vya msingi sana ila kikubwa ni kuwa kuna wakati mtu anakuwa anaogopa kujiuliza maswali magumu. Unaweza kujiuliza nina maanisha nini?

Iko hivi mahusiano ya ndoa ni tofauti sana na mahusiano ya uboifrendi na ugelofrendi 🙃. Ndoa ni muunganiko, ni kiapo,na ni maagano ambayo wawili wanayaingia mbele ya Mungu wanaye muamini kupitia imani zao na mbele ya viongozi wao wa dini na kiroho ili kwenda kuanza maisha pamoja. Kwanini unafikiri Kitendo tu cha Wewe kusema nataka kuoa au kuolewa na mtu fulani kinawafanya wakubwa wako ndani ya familia wakuulize kwanza maswali mengi?Ni kwasababu wanataka walau wa kiwango kidogo wapate kumfahamu huyo mtu hata kwa ufupi kupitia wewe ili kuweza kijiridhisha kuwa unafanya maamuzi sahihi.

Hivyo vyote vinafanyika kukusaidia Wewe ingawa hutoona hivyo kwa wakati huo lakini ndiyo iko hivyo. Maswali wanayokuuliza ni kwasababu wao wanayaishi au hata walikuwa wanayaishi hayo maisha ya ndoa hivyo wanafahamu vitu ambavyo Wewe huvifahamu, na kwasababu wanakujua nje ndani usibishe😊

Sasa nina maanisha nini ninaposema Kama hakujali Kimwili hatokujali Kiroho?

Labda nikwambie tu, mtu wako uliyenaye sasa hivi tabia zake unazifahamu fika na unajua kabisa hii tabia inaweza kuwa ngumu kwake kuacha na hii anaweza akaacha. Sasa kasumba inayo wakumba wengi (hasa wanawake) ni kufumbia macho baadhi ya tabia wakiamini kwamba tukishafunga ndoa atabadilika au nitambadilisha, pia kuna baadhi ya tabia ukiziona wewe mwenyewe unajua hii naweza kuvumilia, hii siwezi ndio maana kabla ndoa haijafungwa huwa unaulizwa Je uko tayari kuolewa na fulani?

Sasa upo kwenye mahusiano na mtu anayekupiga na hata hamjafunga ndoa ni kipi basi kinakufanya uamini kuwa ataacha mkishafunga ndoa?utambadilisha vipi mkishafunga ndoa? Umepigwa mara ya kwanza hujachukua hatua yoyote (hata kiberiti hujakitingisha)unadhani ataacha? Ngoja nikwambie unafahamu vile mtoto anavyomjaribu mzazi wake kwa kufanya kitu sasa mzazi akikaa kimya mtoto naye atasema kumbe hii ni sawa lakini mzazi akisema mtoto nae atajua kuwa hii sio sawa,ndivyo hivyo na wewe unatakiwa uwe. Usipigwe mara ya kwanza ukakaa kimya eti kisa unataka ndoa hapana, mbona yeye humpigi kama mbwa mwizi? Mjaribishe basi kumpiga kama anavyo kudunda wewe kisha muulize vipi unajisikiaje? Huo ni mwili wako inabidi hauheshimu kukutia alama au ukilema wakati kwenu alikutoa huna alama au hicho kilema sio sawa. Usiende kuingia ndani ya ndoa ambayo utaishi kwa kugugumia, kwa kujutia na kwa kulia kila siku kisa unapigwa au unafanyiwa vitendo vingine vya ajabu.

Kama ambavyo Wewe unaujali na kuupenda mwili wako ndivyo vivyo hivyo mwanaume/mume wako anatakiwa aujali pia. Na siku zote mwanaume anayeujali mwili wako atakujali na kiroho. Atakuombea, atakuwa anamshukuru na kumsifu Mungu kwa kumpatia mke ambaye ni wewe. Furaha yake ni kuona mke wake ana Amani, furaha na Afya njema, na ikitokea umeumwa utaona jinsi ambavyo anaongea na Mungu ili afya yako irudi. Na hakuna ndoa tamu kama ndoa ambayo wanandoa huombeana, huwaziana mema, hushirikiana na kujaribu kutatua tatizo pamoja na sio kumuona mwenzako ndio ana tatizo.

Hizi tabia za mwanaume wa namna hii utaziona hata kabla hamjafunga ndoa, mwanaume au mwanamke mwenye hofu ya Mungu ndani yake utamuona tu. Matendo yake yatajifunua kwako. Mema hayajifichi na mabaya huonekana fanya uchaguzi na maamuzi sahihi ili kuepuka kujutia mbele ya safari.🤗

--

--

Lilian Chonya
Lilian Chonya

Written by Lilian Chonya

Karibu usome nakala zangu kuhusu| Mahusiano | Malezi | Ndoa

No responses yet